Wakili wa Sheikh Ponda
DAR ES SALAAM, Tanzania
Wakili wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (54) ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi mpya ya kufanya uchochezi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Nassor Jumaa, amesema kuwa amesikitishwa na hatua ya vyombo vya dola kumuondoa Ponda aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Kitengo cha Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu(MOI) alikokuwa akipatiwa matibabu na kisha kumwamishia katika gereza la Segerea.
Wakili Jumaa alisema amesikitisha na kitendo hicho kwani hakimu Hellen Riwa juzi muda mfupi baada ya wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka kumaliza kumsomea shitaka Ponda, hakimu Liwa alitoa amri ya Ponda aendelee kukaa chini ya ulinzi lakini cha kushangaza leo,wanausalama wamemtoa wodini na kumpeleka katika gereza la Segerea na kwamba atalazimika kurudishwa tena mahakamani siku kesi yake itakapojatwa Agosti 28 mwaka huu, ambapo upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
“Kwa kweli kitendo hicho kime nisikitisha na kunishitua sana ….ila tunatafakari ni hatua gani za kisheria tutazichukua huko siku za usoni’alisema wakili Jumaa.
Agosti 14 mwaka huu, saa kumi jioni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliamia katika wodi hiyo ya MOI na wakili wa serikali Tumaini Kweka alimsomea shitaka Ponda ambaye anakabiliwa na kesi hiyo ya Jinai Na.144 ya mwaka huu.